Tuesday, December 28, 2010

JUKWAA LA SANAA BASATA LAJA NA SURA MPYA 2011

Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego (Kushoto) akielezea masuala mbalimbali yaliyojitokeza kwenye Jukwaa la sanaa katika kipindi cha mwaka unaomalizika mwishoni mwa wiki hii.Katikati ni Mwalimu Komba wa Udsm na Mratibu wa Jukwaa la Sanaa,Ruyembe C.Mulimba
  Mwalimu Komba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Idara ya Sanaa akiwasilisha mada kuhusu Matumizi ya ala katika sanaa ya muziki kwenye Jukwaa la Sanaa,Basata Jumatatu hii

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Ghonche Materego amesema kwamba, kuanzia mapema Januari mwaka 2011 Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu Basata litakuwa na muonekano mpya huku likitoa fursa kwa wasanii kulitumia kama Jukwaa la kutangaza na kuonesha kazi zao.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa la kufunga mwaka wa 2010 Jumatatu hii,Materego alisema kwamba,kwa sasa Jukwaa pamoja na kubeba mada na mafunzo mbalimbali kama ilivyokuwa awali litakuwa wazi kwa wasanii wote wanaotaka kuzindua kazi zao, kuzionyesha kwa wadau, kuziwasilisha (listening event) kabla ya kuzipeleka sokoni na vilevile kuzitambulisha kwa wadau wapana.

“Leo Jukwaa letu la Sanaa linamaliza mwaka,2011 tunadhamiria kuhakikisha sanaa inaweza kuongeza pato binafsi la msanii, kuongeza ajira na kupunguza umaskini wa kipato miongoni mwa wasanii na taifa kwa ujumla.Kwa kuanzia lazima tuanze kwa kuwapa nafasi wasanii kuonesha kazi zao na baadaye kupata mrejesho kutoka kwa wadau” alisema Materego.

Alizidi kufafanua kwamba,wasanii wamekuwa wakipeleka kazi zao sokoni bila kupata wasanii wa kuzijaribu na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali hali ambayo imekuwa kwa kiwango kikubwa ikisababishwa kazi zao zishindwe kufanya vizuri sokoni kutokana na kutoshirikisha wadau mbalimbali.

“Ili kupata nafasi ya kuboresha kazi za wasanii na wao kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wadau, Jukwaa la Sanaa litatoa fursa kwa wasanii kufanya maonyesho katika vipindi mbalimbali na baadaye kuulizwa mawasili, kupokea maoni na michango mbalimbali” alisisitiza Materego.

Akizungumzia mafanikio ya Jukwaa la Sanaa katika kipindi cha mwaka unaomalizika,Materego alisema kwamba, jumla ya mada mbalimbali 43 zimewasilishwa na wawasilishaji 47 ambapo wadau wa tasnia ya sanaa zaidi ya 2,600 wameelimishwa juu ya masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na changamoto mbalimbali zilizoibuliwa kutatuliwa na mamlaka mbalimbali za serikali.Idadi hiyo ya wadau 2,600 iliyohudhuria katika kipindi cha mwaka huu ni zaidi ya malengo kwani lengo lilikuwa ni wadau 1,000.

Alizitaja baadhi ya changamoto ambazo ziliibuka kwenye Jukwaa la Sanaa na kutatuliwa na mamlaka husika kuwa ni pamoja na maadili mabovu ya wasanii katika vipindi vinvyorushwa kwenye runinga,elimu ya sanaa kufundihswa toka ngazi za shule za awali, uboreshaji wa matamasha ya sanaa,uboreshaji wa masoko ya ndani na ya nje kwa kazi za wasanii, urasimishaji wa sekta ya sanaa, matumizi ya lugha miongoni mwa wasanii na kufuatilia pia kudhibiti uvaaji usiofaa wa wasanii hasa wanenguaji kwenye majukwaa.

“Masuala kama elimu ya sanaa kutolewa kuanzia ngazi ya shule za awali,uboreshaji wa sanaa zetu, usimamizi thabiti wa matamasha ya sanaa, uboreshaji wa masoko ya ndani na ya nje yako kwenye mpango mkakati wa BASATA wa mwaka 2011-2014.Pia ninaamini sheria ya hakimiliki na hakishiriki iliyo chini ya Cosota katika bunge hili itajadiliwa na kupitishwa rasmi” alimalizia Materego huku akitoa pongezi kwa wadau wa sanaa wote waliohudhuria katika kipindi cha mwaka unaomalizika.

Awali kabla ya Materego kuongea,Mwalimu Komba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Idara ya Sanaa alitoa elimu juu ya Matumizi ya ala katika sanaa ya muziki ambapo alitoa wito kwa wasanii kuingia darasani na kujifunza matumizi ya ala za muziki hasa zile za asili badala ya wao kuwa waimbaji pasi na kutumia ala.

Jukwaa la Sanaa litaendelea tena wiki ijayo (Jumatatu ya Januari 3, 2011) ambapo Mratibu wa onyesho maarufu la kila mwaka la Sauti za Busara,Kwame Mchauru atawasilisha mada itakayohusu ‘Mchango wa Matamasha ya Sanaa Katika Kuongeza Ajira na Pato nchini Tanzania’.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU