Tuesday, January 4, 2011

BASATA YAJA NA TAMASHA LA SIKU YA MSANII WA TANZANIA


Aliyekuwa Mratibu Msaidizi wa Tamasha la Sauti za Busara linalofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar,Kwame Mchauru (Katikati) akiwaeleza wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya mchango wa matamasha katika kutao ajita nchini Tanzania.
  Msanii wa kizazi kipya,Symon John aka Gheto King akimuuliza Mratibu wa Tamasha la Sauti za Busara jinsi ya kuwawezesha wasanii kushiriki kwenye tamasha hilo
Wadau wakifuatilia kwa makini Jukwaa la Kwanza la Sanaa.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) baadaye mwaka huu litaandaa tamasha kubwa la wasanii ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka likiwa na jina la siku ya msanii wa Tanzania.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika katika ukumbi wa baraza hilo kila Jumatatu,Katibu Mtendaji wake Ghonche Materego alisema kwamba,tamasha hilo ambalo litakuwa likipambwa na burudani kemkem kutoka kwa wasanii wa sanaa mbalimbali  hapa nchini litakuwa ni maalum kwa ajili ya kuenzi sanaa na kusisitiza kaulimbiu ya sanaa ni kazi kwa vitendo.

“Katika kuhakikisha sanaa inakuwa kweli kazi na ajira kama ilivyo kaulimbiu yetu mwaka huu,watendaji wa BASATA wako katika maandalizi ya kuandaa tamasha la siku ya wasanii ambalo tutawapa taarifa zake hivi karibuni.Katika tamasha hilo wasanii wetu watapata fursa za kuonyesha kazi zao na kushiriki kikamilifu” alisema Materego.
Aliongeza kwamba,tamasha hilo litakuwa ni mwanzo wa kuenzi wasanii wetu na kukuza sekta ya sanaa nchini hasa ikizingatiwa itakuwa ni fursa kwa wasanii kujitangaza na kupanua mwanya wa masoko ya kazi zao.

Huku akiomba ushirikiano wa dhati kutoka kwa wadau mbalimbali hasa wale wa sanaa,Materego aliongeza “Tunataka wasanii wetu sasa waone faida ya kazi zao,wazalishe sanaa zenye ubora na zinazoweza kukubalika na kuvuta watu wengi.Hii ndiyo siri pekee ya kuwafanya wapate fursa ya kushiriki maonyesho na matamasha mbalimbali ya sanaa ndani na nje ya nchi lakini pia kufanya kazi zao ziuzike”.

Awali akiwasilisha mada katika Jukwaa la Sanaa,iliyohusu Mchango wa Matamasha ya Sanaa Katika Kukuza Ajira nchini Tanzania,aliyekuwa Mratibu Msaidizi wa onyesho maarufu hapa nchini la Sauti za Busara,Kwame Mchauru alisema kwamba, wasanii hawana budi kutengeneza sanaa zenye ubora na zenye asili ya Tanzania ili kuweza kupata fursa ya kushiriki maonyesho na matamasha mbalimbali ya ndani na nje ya nchini.

Aliongeza kwamba, matamasha na maonyesho ya kazi za sanaa ndiyo daraja kubwa la mafanikio kwa wasanii hivyo hawana budi kusaka fursa za kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kazi zao zinakuwa na ubora unaohitajika kwani hicho ndicho kigezo kikubwa cha kuwawezesha kushiriki.


0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU