Tuesday, March 27, 2012

BASATA: UKIUKWAJI WA MAADILI KATIKA SANAA SASA BASI

 Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza hilo ambapo mada ya wiki hii ilihusu Sanaa ya Unenguaji na Maleba katika Muziki. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Juma Ubao na Mtendaji wa Binti Leo, Betty Kazimbaya.
 Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Bw. Ubao akieleza athari za kuwepo kwa unenguaji usiyozingatia maadili kwenye muziki wa dansi wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
  Mtendaji kutoka asasi ya Sanaa za Majukwaani ya Binti Leo Bi. Betty Kazimbaya akiongea na Wadau wa Sanaa kuhusu Umuhimu wa Maleba Kwa Wasanii wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa.Kulia ni Mratibu wa Jukwaa hilo, Godfrey Lebejo.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala.
Baraza la Sanaa la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kukerwa na hali ya uvunjifu wa maadili katika sanaa hususan unenguaji na kutaka hali hiyo sasa ifike mwisho.

Akizungumza katika Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Ghonche Materego alisema kuwa, ni lazima kuwe na mabadiliko dhidi ya uvunjifu maadili kwenye sekta ya Sanaa vinginevyo hatua zitaanza kuchukuliwa.
“Haya si mambo yanayofurahisha, ni lazima jamii ioneshe ushirikiano kwa kupambana na udhalilishaji wa aina hii, kuna mambo yasiyopaswa kufanyika hadharani na yanabaki kuwa ya ndani tu kwenye night club na Casino na si vinginevyo” alisistiza Materego.

Aliongeza kuwa, haivumiliki kwa maonesho hayo ya sehemu maalum za ndani kuanza kufanywa hadharani kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi na ni udhalilishaji wa sekta ya Sanaa hivyo aliwataka Wasanii kujipanga kupiga vita hali hii.
“Mabadiliko lazima yafanywe. Vyama, mashirikisho na mitandao ya Wasanii vianze mara moja kuangalia maadili kwenye maeneo yao. Hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya watakaoendelea kuvunja maadili kwenye Sanaa” alizidi kusisitiza Materego.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) Juma Ubao alisema kuwa, kinachofanyika sasa kwenye unenguaji si muziki wa dansi bali ni aina fulani ya matukio ambayo ni maalum kwa ajili ya night club na kasino.
“Unenguaji wa uchi usihusishwe hata kidodo na muziki wa dansi. Haya yanayofanyika sasa ni kuuchafua muziki huu. Ni lazima tuelewe haya si ya kuvumilia kwenye muziki wetu” alisisitiza Ubao.
Alizidi kueleza kuwa, huko nyuma wanenguaji walivaa kwa heshima na kufanya maonesho yaliyovutia watu wa rika zote lakini kwa sasa hali ni tofauti kutokana na kuwepo kwa vikundi vinavyovaa uchi na kuanza kunengua hadharani.
Kwa upande wake, Mtendaji kutoka asasi ya Binti Leo inayojishughulisha na Sanaa za majukwani Bi. Betty Kazimbaya alisema kuwa, kinachofanyika sasa ni kudhalilisha Sanaa na ukiukwaji wa maadili kupitia maleba (mavazi ya Wasanii) hivyo kutaka hatua zichukuliwe.
“Kazi kubwa ya maleba (mavazi ya wasanii) ni kusitiri mwili, inakuaje kuwe na vikundi havitumii mavazi haya kwa kazi hiyo? Alihoji Kazimbaya.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU