Tuesday, July 31, 2012

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SIREFA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 28 mwaka huu.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SIREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Singida.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya SIREFA chini ya uenyekiti wa Baltazar Kimario ambaye amechaguliwa kwa mara ya kwanza.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Singida kwa kuzingatia katiba ya SIREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya SIREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Singida ni Baltazar Kimario (Mwenyekiti), Hussein Mwamba (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Gabriel Mwanga (Mhazini), Hamisi Kitila (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Salum (Mwakilishi wa Klabu TFF), Yagi Kiaratu na Dafi Dafi (wajumbe wa Kamati ya Utendaji).

Nafasi za Makamu Mwenyekiti, Mhazini Msaidizi na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji zitajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye.

MICHELSEN AITA 22 KAMBI YA COCA-COLA
Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini. Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu.

Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi).

Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma).

Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU