Kocha wa Azam anayerudishwa Stewart Hall
Kocha aliefukuzwa Boris Bunjak
KOCHA Mserbia wa Azam FC, Boris
Bunjak amefukuzwa rasmi leo na sasa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Muingereza
Stewart Hall anarudishwa kazini.
Habari kutoka ndani ya Azam FC
zimesema kwamba, sababu za kufukuzwa kwa Mserbia huyo ni kushuka kwa kiwango
cha timu, hali iliyosababisha sasa ianguke hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa
Ligi Kuu.
Tayari Bunjak amekwishapewa haki
zake zote na ataondoka Alhamisi, siku ambayo Stewart atawasili kuanza tena kazi
Azam FC.
Bunjak anaondoka Azam baada ya
kuiongoza timu katika mechi 16, akifungwa nne tu, zote dhidi ya Simba ikiwemo
ya juzi ya Ligi Kuu, waliyofungwa 3-1 na kutoa sare tatu
Bunjak mwenye leseni ya Shirikisho
la Soka Ulaya (UEFA), alitua Azam, Agosti 7, mwaka huu akitokea FC Damac ya
Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na kabla ya hapo alifundisha
klabu kibao za kwao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK Javor Ivanjica, Crvena
Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK Mladi Radnik, FK Crvena
Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali, Bunjak aliyezaliwa Novemba
17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika klabu za FK Sloga (Kraljevo),
FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac), FK Olimpia (Ljubljana), FK
Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK Borac (Cacak) na FK Sloga
(Kraljevo).
Stewart alifukuzwa kwa kosa la
kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan
Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame dhidi ya Yanga.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano
kufukuzwa Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada
ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin,
Mbrazil mwingine.
Lakini Stewart angalau aliacha
kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la
Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya
kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame miezi miwili iliyopita, mambo
ambayo bila shaka yamemfanya afikiriwe tena.
0 maoni:
Post a Comment