Tuesday, October 30, 2012

KAMBI YA REDDS MISS TANZANIA YAZUA HOFU

WAKATI zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya Redd’s Miss Tanzania 2012 kupatikana, mambo ndani ya kambi ya warembo 30 wanaowania taji hilo imekuwa ya hofu tupu, huku kila mshiriki akibaki kujiuliza nani atatwaa taji hilo.
 
Miss Redd’s Tanzania 2012 atajiwalia gari pamoja na fedha taslimu Sh milioni 8, katika kinyang’anyiro kinachotarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl uliopo jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam siku ya Jumamosi.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kambi ya timu hiyo iliyopo hoteli ya Giraffe, Kunduchi, Dar es Salaam warembo mbalimbali walisema washiriki wote kwa sasa wana hofu tupu.
 
“Pamoja na kuingia 15 bora ya Redd’s Miss Tanzania mpaka sasa, lakini bado sina uhakika kama nitatwaa taji, maana kila mrembo namuona yuko bomba,” alisema Redd’s Miss Photogenic, Lucy Stephano.
 
Mpaka sasa washiriki watatu waliofanikiwa kuingia hatua ya 15 bora ni Lucy pamoja na Mary Chizi aliyetwaa taji la Miss Sports Lady na Babylove Kalala aliyefanikiwa kushinda lile la Redd’s Miss Talent.
 
Warembo hao wawili pia walizungumzia ugumu wa shindano hilo, huku Mary akisema kuna kazi kubwa na Babylove akidai kila kitu kwa sasa amekiacha mikononi mwa Mungu.
 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency, Hashim Lundenga, ambao ndio waandaaji wa shindano hilo alisema, kila kitu kwa sasa kimekamilika na wana imani kubwa shindano litakuwa kali na la kuvutia.
 
“Tumekamilisha kila kitu, naamini atapatikana mrembo mkali zaidi ambaye atatuwakilisha vema katika mashindano ya dunia,” alisema.
 
Naye Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original walio wadhamini wakuu wa shindano hilo, Victoria Kimaro, alisema huu ni wakati sahihi wa kumpata mshindi bomba mwenye vigezo.
 
“Kwa jinsi mambo yalivyo, nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi siku ya shindano, maana hili litakuwa ni shindano la kipekee,” alisema.
 
Shindano hili la Redds Miss Tanzania 2012 linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji cha Redds Original.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU