Wednesday, October 10, 2012

CASTLE LAGER SUPERFANS' SASA LAFIKA PATAMU

 
SHINDANO la kumsaka shabiki bora wa Ligi Kuu ya England, maarufu zaidi kwa jina la ‘Castle Lager Superfans’ kwa sasa limefika patamu na washindi sita waliopatikana wanatarajiwa kutangazwa Jumatatu ijayo.
 
Shindano hilo linaendeshwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Castle Lager ambao pia ni wadhamini wenza wa Ligi Kuu ya England.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Castle Lager, Kabula Nshimo alisema mchujo wa mashabiki hao ulikuwa mgumu kutokana na watu wengi kujitokeza.
 
Kabula alisema, jumla ya mashabiki 361 walijitokeza kwa kutuma picha zao katika mtandao wa kijamii wa Facebook na promosheni walizoziendesha katika mikoa mbalimbali.
 
Meneja huyo alisema, baada ya mchujo walipatikana washindi 32 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, ambao walipigiwa kura na kupatikana 15.
 
“Katika hao 15 ndio ambao walifanyiwa mahojiano ya ana kwa ana , hivyo wamechujwa na kupatikana sita, ambapo watasakwa washindi wawili ili waunde timu ya Castle Lager Superfans Tanzania,” alisema.
 
Washindi hao sita wanatarajiwa kutangazwa Jumatatu ijayo, ambapo watazunguka nchi nzima ili kuomba kura kutoka kwa mashabiki wa Ligi Kuu England.
 
Kabula alisema washindi hao wawili watakaopatikana, wataungana na wengine kutoka Swaziland, Zambia, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kuunda timu ya ushangiliaji itakayogharamiwa kila kitu katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika hapo mwakani. Fainali hizo zitafanyika Afrika Kusini.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU