Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
vifo vya wachezaji watano wa timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera
vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka huu).
Rusumo
FC ilikuwa ikitoka kwenye mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya
Ngara ambapo ikiwa njiani kurudi Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali
ya gari na wachezaji watano kufariki papo hapo.
Wachezaji wengine ambao ni majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao zikiwa mbaya.
Msiba
huo ni pigo kwa familia za marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha
Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Kagera (KRFA) na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na
mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa mchezo huu kupitia klabu yao.
TFF
inatoa pole kwa familia za marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na
kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito.
Kutokana
na msiba huo, mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa leo
(Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na dakika moja ya maombolezo ili kutoa
heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema
peponi. Amina
0 maoni:
Post a Comment