Thursday, October 25, 2012

TASWA YAMPONGEZA WAMBURA

A: Pongezi Wambura
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinampongeza mwanachama wake Boniface Wambura kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
TASWA imepokea kwa furaha uteuzi huo wa Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na inaamini ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake ya kazi ndani ya TFF.

Tangu Wambura aanze kazi ya Ofisa Habari wa TFF kumekuwa na mapinduzi makubwa yanayohusiana na mambo ya habari na katika hili waandishi wa habari za michezo nchini ni mashahidi wa hilo kwani amekuwa mtu sahihi kwao na amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na kifani kwa wanahabari wenzake.

Kwa vile Wambura ni mwanachama wetu hai wa TASWA, kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na tunamtakia kila la heri ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni ishara tosha kwamba kazi yake inaonekana na inathamanika.
Wambura ameteuliwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012, ambapo atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.

B: Mkutano Mkuu wa TASWA
Sekretarieti ya TASWA imefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.

Kamati ya Utendaji ya TASWA ilikubaliana katika kikao chake mwezi uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa TASWA mwaka huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha wanachama kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na ikashauri ikiwezekana ufanyike nje ya Dar es Salaam kama hali itaruhusu.

Kutokana na hali hiyo, kikao kiliiagiza sekretarieti ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala hilo na kwamba kama ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe na mdhamini.

Tayari hilo limefanyika na mdhamini amepatikana, ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema wiki ijayo  na baada ya hapo itatangazwa tarehe rasmi.
Nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili waepuke usumbufu wa kushindwa kuhudhuria mkutano huo.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU