Monday, December 17, 2012

SITA ZATINGA ROBO FAINALI UHAI CUP


Timu sita zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 (U20) wa klabu za Ligi Kuu ya Tanzania.

Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayofanyika viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam na kudhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitai maji Uhai itafanyika Desemba 19 mwaka huu kwenye viwanja hivyo hivyo.

Timu zilizofuzu kutoka kundi  A ni Coastal Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro na JKT Ruvu ya Dar es Salaam. Kundi C ni Oljoro JKT ya Arusha na Ruvu Shooting ya Pwani wakati iliyofuzu kutoka kundi A hadi sasa ni Azam pekee.

Katika mechi zilizochezwa leo asubuhi (Desemba 17 mwaka huu) Coastal Union na Mtibwa Sugar zimetoka suluhu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, wakati Uwanja wa Azam ulishuhudia African Lyon ikiifunga Mgambo Shooting mabao 2-1.

Nafasi mbili za robo fainali zilizobaki kutoka kundi B zinawaniwa na timu za Simba, African Lyon na Polisi Morogoro. Mechi itakayochezwa leo saa 10 jioni katika Uwanja wa Chamazi kati ya Polisi Morogoro na Simba ndiyo itakayoamua timu zitakazoungana na Azam kutoka kundi hilo.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU