Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye
mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur
Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo
kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa
habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya
mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa
ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na
mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya
kutoa tamko.
“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA.
Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri,
hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa
Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata
uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano
yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni
wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa
yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae
mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano
hayo.
Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la
Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA
iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano
hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama
wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia
kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu
ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya
kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri
tamko la Serikali,” alisema Tenga.
“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa
uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu
Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki
nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.
Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu
ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi
ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali
kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema
Tenga.
“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali
taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa
tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa
tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka
serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua
mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho
kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo
hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao
mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia
CECAFA usalama,” alisema.
“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si
nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje
ya CECAFA.”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 maoni:
Post a Comment