Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa
Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye
vizuri katika mechi yake ya kesho (Juni 8 mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini
Marrakech.
Stars, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye
kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast
kwa tofauti ya pointi moja, inacheza na Morocco katika mechi ya nne
itakayofanyika Marrakech baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi
ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Machi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Rais wa TFF,
Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata
udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa
miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.
“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata
udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga
kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.
“Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL
ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho
za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri;
kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata
kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).
“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara
mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na
udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”
Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza
kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya
muda mrefu.
“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na
tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu
wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.
Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais
Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema
kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe
alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano
baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.
Katika mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi
ya Jamii (NSSF) lilikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda
Morocco kuishangilia timu.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu
alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine
zilitarajiwa kusafirishwa jana.
0 maoni:
Post a Comment