Tuesday, September 10, 2013

KIMONDO KUCHEZA MBOZI, KURUGENZI WAMBI FDL

Timu za Kimondo SC ya Mbeya na Kurugenzi ya Mafinga zitatumia viwanja vya Mbozi na Mafinga kwa ajili ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza Jumamosi (Septemba 14 mwaka huu).

Kimondo SC sasa itatumia Uwanja wa CCM Vwava ulioko wilayani Mbozi badala ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine wa jijini Mbeya. Nayo Kurugenzi itatumia Uwanja wa Wambi ulioko Mafinga mkoani Iringa badala ya Uwanja wa Makambako ulioko mkoani Njombe.

Mechi za fungua dimba FDL msimu huu zitakuwa kati ya Burkina Faso na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, Mkamba Rangers na Lipuli ya Iringa kwenye Uwanja wa CCM Mkamba, Majimaji na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Kimondo na Kurugenzi kwenye Uwanja wa CCM Vwawa katika mechi za kundi B.

Septemba 14 mwaka huu Tessema na Green Warriors zitaoneshana kazi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Siku inayofuata (Septemba 15 mwaka huu) Transit Camp na Polisi Dar (Mabatini mjini Mlandizi) wakati mechi nyingine za kundi hilo la A zitakuwa kati ya Villa Squad na African Lyon (Karume) na Ndanda FC na Friends Rangers (Nangwanda Sijaona, Mtwara).

Kundi C ni Polisi Mara na Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT na Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United na Mwadui (Kambarage, Shinyanga) wakati Pamba na Toto Africans zitamenyana Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

PONDAMALI AFUNGIWA MIEZI 3, FAINI MILIONI 1/-
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. milioni moja na kumfungia miezi mitatu kocha wa makipa wa timu ya Coastal Union kwa kuwatukana washabiki wanaominika kuwa wa Simba.
Pondamali alifanya kosa hilo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mwamuzi Martin Saanya na mwamuzi msaidizi namba moja Jesse Erasmo waliochezesha mechi kati ya Yanga na Coastal Union nao wamefungiwa mwaka mmoja kila mmoja kwa kutoimudu mechi hiyo.

Nayo Yanga imepigwa faini ya sh. milioni moja (sh. 500,000) kwa kila kosa kutokana na washabiki wake kuwarushia waamuzi chupa za maji baada ya Coastal Union kusawazisha bao katika mechi hiyo. Pia waliwarushia chupa waamuzi hao wakati wakirejea vyumbani baada ya pambano hilo.

Vilevile Coastal Union imepigwa faini ya sh. 100,000 baada ya kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Timu hiyo ilichelewa kwa dakika 23. Kikao kinatakiwa kuanza saa 4 kamili asubuhi.

TEMEKE YAIZAMISHA RUKWA 5-1 COPA COCA-COLA
Temeke imejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza robo fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo (Septemba 10 mwaka huu) asubuhi kuizamisha Rukwa mabao 5-1.

Hadi mapumziko katika mechi hiyo ya kundi B hatua ya Fainali za Taifa iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, washindi walikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao ya washindi yalitiwa wavuni na Constantine Katepa aliyefunga dakika ya 28, Patrick Ambrose dakika ya 36 huku Hamisi Kajole akipiga mawili dakika ya 43 na 71. Bao la nne lilifungwa dakika ya 46 na Ramadhan Juma.

Rukwa ambayo kwa matokeo hayo imeshatolewa ilipata bao lake dakika ya 51 kupitia kwa Francisco Nkanga. Timu nyingine katika kundi hilo ni Geita na Ilala.

Robo Fainali ya michuano hiyo itaanza keshokutwa (Septemba 12 mwaka huu). Kila kundi linatoa timu mbili kucheza hatua hiyo katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Coca-Cola.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU