Thursday, November 28, 2013

KUMEKUCHA MBIO NDEFU ZA UHURU MARATHON

Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini, Suleiman Nyambui (Kulia), akimkabidhi fomu ya ushiriki wa mbio za kilomita 3 za Uhuru Marathon,mwanamichezo Imani Madega (Kushoto), huku mratibu wa mbio hizo,Innocent Melleck akishuhudia wakati wa tukio la kuonyesha njia mbio hizo zitakazoshirikisha watu wa rika tofauti na viongozi mbalimbali zitakavyokuwa kwenye viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Mbio hizo ambazo lengo lake ni kuhamasisha umuhimu wa uwepo wa amani nchini zitafanyika Desemba 9 mwaka huu.

KUMEKUCHA! Mbio ndefu za Uhuru, Uhuru Marathon, sasa zimefikia patamu baada ya waandaaji jana kutangaza njia itakayotumika kwa ajili ya mbio hizo.
 
Mbio za Uhuru Marathon zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Desemba 8, mwaka huu na zitaanzia viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni na kumalizikia hapo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Selemani Nyambui alisema, njia hizo zimepimwa kwa kuzingatia taratibu zote za mbio za kimataifa.
 
Nyambui alisema, upimaji ulifanyika kwa umakini mkubwa kwa kuhakikisha wale watakaokimbia mbio za kilomita 42, kilomita 21 na kilomita 5 wanakimbia kwa kiwango sahihi zaidi.
 
Nyambui alitaja njia zitakazotumika kwa wanariadha wa kilomita 42 kuwa, wataanzia Viwanja vya Leaders na kupitia Barabara ya Alli Hassan Mwinyi kuelekea Morocco, watapitia Old Bagamoyo kuelekea Kawe na kufuata barabara ya Tegeta.
 
Wanariadha hao watapita pia Mwenge hadi Makumbusho ambapo watafika eneo la Morocco na kuchukua Barabara ya Kawawa hadi katika taa za Chang’ombe, ambapo wataelekea Tazara na wakifika hapo watafuata Barabara ya Mandela hadi Uwanja wa Taifa.
 
Wakifika hapo watapita Barabara ya Taifa na kutokea Chang’ombe na kwenda hadi Kinondoni kwa Manyanya watakapochukua barabara ya kuelekea makaburini (Kinondoni Road) na kutoka Barabara ya Alli Hassan Mwinyi na hatimaye kuingia Viwanja vya Leaders.
 
Nyambui alisema, mbio za kilomita 21 zitatumia njia hizo lakini lakini hazitafika eneo la Chang’ombe kama ilivyo kwa zile za kilomita tano.
 
“Naamini kwa dhati kabisa mbio hizi zitafanikiwa kwa kiasi kikubwa na mpaka sasa wanariadha wengi wamejitokeza kushiriki,” alisema.
 
Naye Katibu wa Kamati ya mbio hizo, Innocent Melleck alisema, wanaamini kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa haswa kwa mipango waliyoiweka.
 
Melleck alisema, mpaka sasa usajili unaendelea ambapo kwa wa kilomita 3 atalipa Sh 100,000 yule wa kilomita 5 Sh 2,000 na washiriki wa kilomita 21 na 42 watalipia Sh 6,000.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU