Kamati
ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia mechi tatu
wachezaji watano kati ya tisa wa timu ya Kanembwa JKT waliolalamikiwa na
Sekretarieti kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyochezwa
Novemba 2 mwaka jana.
Wachezaji
hao ni Bariki Abdul, Mrisho Musa, Nkuba Clement, Nteze Raymond na Philo Ndonde.
Wachezaji ambao hawakutiwa hatiani kutokana na ushahidi dhidi yao
kutojitosheleza ni Abdallah Mgonja, Mbeke Mbeke, Ntilakigwa Hussein na Uhuru
Mwambungu.
Mechi
hiyo dhidi ya Stand United iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga
ilivunjwa na refa Peter Mujaya dakika ya 87 kutokana na kupigwa na wachezaji
hao baada ya kuamuru ipigwe penalti dhidi ya timu yao.
Adhabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 49 (1)(b) ya Kanuni za Nidhamu za TFF
baada ya kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na Sekretarieti ya TFF ambavyo ni
ripoti ya refa, ripoti ya kamishna wa mechi hiyo na video iliyoonesha tukio
hilo.
Pia
kabla ya kutoa adhabu baada ya kusikiliza utetezi kutoka kwa walalamikiwa ambao
ni wachezaji hao na timu yenyewe ya Kanembwa JKT. Nayo Kanembwa JKT imetiwa
hatiani na kupigwa faini ya sh. milioni ambayo inatakiwa kuilipa kabla ya
kucheza mechi inayofuata.
Kamati
hiyo iliyokutana jana (Februari 9 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba
Abbas, kwanza imelaani kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kumzonga refa, kwani vitendo
vya aina hiyo ndiyo vichocheo vya vurugu viwanjani.
Lakini
pia imempongeza nahodha wa Kanembwa JKT, Mbeke Mbeke kwa kuwa mstari wa mbele
kuwazuia wachezaji wenzake waliokuwa wakimpiga refa wa mchezo huo.
Vilevile
Kamati hiyo imesema aliyesababisha matatizo hayo ni refa Mujaya, na ingawa
ilikuwa na uwezo wa kumchukulia hatua lakini haikufanya hivyo kwa vile hakukuwa
na mlalamikaji na tayari Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilishamwadhibu.
MAJINA YA
MABINGWA WA MIKOA MACHI 30
Vyama
vya Mpira wa Miguu vya mikoa vimetakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao
kufikia Machi 30 mwaka huu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Timu
zote zitakazofuzu kucheza RCL zinaruhusiwa kusajili wachezaji wapya wasiozidi
watano kutoka ndani ya mkoa kwa kufanya taratibu za uhamisho. Kamati
imesisitiza kuwa usajili wa RCL ni uleule uliotumika kwenye Ligi ya Mkoa.
Kamati
ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
Februari 6 mwaka huu imekataa ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza
(MZFA) kuongeza timu za Ligi ya Mkoa kutoka 20 hadi 24.
Ikiwa
chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange, Kamati hiyo imesema kwa mujibu wa
Kanuni ya Ligi ya Mkoa, ligi hiyo inatakiwa kuwa na timu kati ya 16 na 20,
hivyo vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vinatakiwa kuendesha ligi kwa kufuata
kanuni.
Kamati
hiyo imeongeza kuwa hata kama ingekubalia ombi la MZFA kiutaratibu lisingewezekana
kwa vile kanuni hufanyiwa marekebisho baada ya msimu kumalizika, wakati ombi
hilo limewasilishwa katikati ya msimu.
KOCHA MARSH
ASUBIRI VIPIMO VYA MWISHO
Kocha
Msaidizi wa Taifa Stars, Sylvester Marsh ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) anasubiri vipimo vya mwisho ili aweze kuanza matibabu.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtoa kocha huyo nyumbani kwake jijini
Mwanza na kumleta Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha anapata matibabu zaidi
na kwa uangalizi wa karibu.
Tayari
majibu ya kipimo cha kwanza yameshapatikana, hivyo yanasubiriwa majibu ya
kipimo kingine ili aweze kuanza rasmi matibabu, lengo likiwa ni kubaini
kitaalamu ugonjwa unaomsumbua.
KIKOSI CHA TWIGA
STARS KUAGWA FEB 12
Timu
ya Twiga Stars itaagwa rasmi Jumatano (Februari 12 mwaka huu) tayari kwa safari
ya Lusaka, Zambia kwa ajili ya mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu
nchini Namibia.
Msafara
wa timu hiyo itakayoondoka kwa ndege ya Fastjet utaongozwa na mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd Mgoyi.
Hafla
ya kuwaaga wachezaji wa timu hiyo itafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.
Timu hiyo itaondoka Februari 13 mwaka huu alfajiri tayari kwa mechi hiyo
itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda.
0 maoni:
Post a Comment