Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu nchini, Wilson Makubi akitaka kujua masuala mbalimbali juu ya Mtandao wa Arterial kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Materego (aliyesimama) akijibu moja ya hoja zilizoibuka kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza hilo. Wengine kushoto kwake ni Bw. Kipeja na Hassan Bumbuli katibu wa CAJAtz.
Katibu wa Mtandao wa Arterial Tanzania, Hassan Bumbuli (Kulia) akionesha moja ya vipeperushi vyenye taarifa mbalimbali kuhusu mtandao wa Arterial kwenye Jukwaa la Sanaa.
Na Mwandishi WetuWasanii wa Tanzania sasa wataunganishwa na wenzao wa Afrika kupitia mtandao wa Arterial ambao kwa mujibu wa wawakilishi wake hapa nchini utakuwa na manufaa makubwa.
Akizungumza wiki hii katika Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz), Mwenyekiti wa mtandao huo hapa nchini Laurian Kipeja alisema kwamba, mtandao huo kwa sasa unawanufaisha wasanii wengi barani Afrika.
“Mtandao huu umeanzishwa rasmi huko Senegal mwaka 2007, kwa sasa umesambaa nchi nyingi za Afrika zikiwemo za Afrika Mashariki. Umewaweka pamoja wasanii wengi na kuwapa wasanii mafanikio” alisema Kipeja.
Aliyataja mafanikio ambayo wasanii watapata kwa kuwa ndani ya mtandao huo kuwa ni pamoja na kukutana na wasanii mbalimbali wa kiafrika, kupata fursa za kushiriki matukio mbalimbali ya kisanaa, kukuza na kuuza kazi zao, kupata elimu juu ya ukuzaji wa stadi zao na faida nyingine nyingi.
“Tunatoa wito kwa wasanii hapa nchini kutumia fursa hii ya kujiunga na Mtandao wa Arterial, faida zake ni nyingi, wenzetu wa nchi za Afrika wameanza kunufaika hivyo ni muda wa wasanii wa Tanzania kuchangamkia fursa hii ya pekee” aliongeza Mwenyekiti huyo wa Arterial mtandao ambao kwa hapa nchini umeanzishwa rasmi Februari 22,2011.
Aidha, Kipeja alitaja kazi ambazo hadi sasa zimefanywa na mtandao huo hapa nchini ambazo ni pamoja na kuandaa vitabu vya Marketing of Art na Fundraising in Art ambavyo muda wowote vitatua nchini kutoka Afrika Kusini, kuandaa semina na warsha mbalimbali kwa wasanii barani Afrika na sasa kuwa na mtandao huo katika nchi za Afrika Mashariki.
Alimalizia kwa kuwashauri wasanii kuwa na barua pepe na kuhakikisha mara kwa mara wanatembelea mitandao ya arterianetwork.com na ule wa artsinafrica.com ambayo kwa pamoja imejaa taarifa mbalimbali kuhusu sanaa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kwamba, kazi za wasanii wa Tanzania zina ubora kuliko zile za nchi nyingine za Afrika Mashariki lakini tatizo limekuwa kwa wasanii wenyewe kujiamini na kuthubutu katika kazi zao.
“Ukizunguka nchi za Afrika Mashariki kumejaa filamu na kazi za sanaa kutoka Tanzania. Zinakubalika kuliko za nchi zingine, tatizo ni kwamba wasanii wetu hawajiamini na kuthubutu. Hapa ndipo wanapotakiwa kubadilika” alisisitiza Materego
0 maoni:
Post a Comment