Tuesday, February 26, 2013

MWAMUZI FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL

Mwamuzi Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.

Waamuzi wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar).  

Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).

Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.

MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.

Kamishna Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.

Makamishna wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF.

Kwa upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.

Wengine ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.

Kamati ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.

KAMATI YA UTENDAJI TFF KUJADILI TAMKO LA SERIKALI
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo la 2012.

Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.

Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU